Tunaendelea na daftari la nne ambalo Mtakatifu Faustina alilijaza tafakari na mafunuo kutoka kwa Yesu. Tunapoanza kusoma daftari hili, jipe nafasi ya kumtafuta Mungu katika ukimya. Sura hii inaanza kwa Mtakatifu Faustina kueleza kwamba alikuwa akipitia “usiku wa giza” (Shajara #1235). Hakuhisi ukaribu wa Mungu kwa hisi zake. Kwa mfano, ingekuwa kana kwamba ulikuwa katika chumba chenye giza kilichojaa hazina, na mtu akakuambia kwamba hazina zote za chumba hicho zilikuwa zako. Hukuweza kuziona, lakini ulimwamini yule aliyekuambia kuhusu vyote vilivyokuzunguka. Ufahamu wa hazina hizi uliijaza akili yako, ingawa giza lilizificha machoni pako.
Ndivyo ilivyo pia katika uhusiano wetu na Mungu. Mtakatifu Faustina alimpenda Bwana wetu kwa moyo wake wote na kwa kila mpigo wa moyo wake. Aliujua ukaribu na upendo Wake. Lakini inaonekana kwamba hakuweza kutambua hayo kwa hisi zake za kibinadamu. Zawadi hii ya giza ilimwezesha kuingia katika uhusiano na Mungu katika kina cha kiroho kilicho kikubwa zaidi.
Tafuta kina hiki cha uhusiano na Mungu unaposoma sura hii. Usiishie kwenye tamaa ya kuhisi kuwa karibu na Mungu, bali jipe nafasi ya kuwa karibu na Mungu. Anataka kuingia moyoni mwako kwa kina kikubwa zaidi kuliko ulivyowahi kufikiri kuwa inawezekana. Uwe tayari kupokea upya wa uhusiano uliofunikwa na giza, na umruhusu Bwana akujulishe Huruma Yake katika kina hiki kipya cha upendo.
Tafakari ya 237: Giza la Imani Hutakasa Upendo Wetu
Watakatifu wengi wakuu, akiwemo Mtakatifu Faustina, walipitia giza la ndani katika uhusiano wao na Mungu. Hali hii ina fumbo kubwa. Kadiri nafsi inavyozidi kuwa karibu sana na Mungu, hupokea faraja nyingi na hisia za upendo katika safari hiyo. Hata hivyo, hufika wakati katika safari ya kiroho ambapo Mungu hujificha. Hili halitokani na dhambi yoyote ya mtu huyo; bali ni njia ya Mungu ya kuingia kwa kina zaidi katika maisha yake ili amtegemeze bila msaada wa faraja ya kihisia au hata ya kiroho. Nafsi hutumbukizwa katika giza linaloweza kuwa lenye maumivu makali. Lakini katika giza hili, mtu hualikwa kumjua Mungu kwa ukimya mpya na kujisalimisha Kwake kwa namna mpya. Yale ambayo nafsi hujulishwa katika kina hiki kipya yanazidi maneno na uzoefu wa kibinadamu. Kuna kumjua Mungu na Mapenzi Yake ya Kimungu, lakini hakuna kumhisi Yeye. Kupitia giza hili, nafsi hualikwa kumchagua Mungu na Mapenzi Yake licha ya kutokuwapo kwa hisia zozote au faraja za kiroho (Tazama Shajara #1235).
Yaelekea maisha yako ya sala bado hayajakufikisha katika hali hii ya giza. Lakini ingawa ni wachache wanaoingia katika kina hiki cha ushirika na Mungu, ni vizuri kukifahamu na kuelewa hali waliyopitia watakatifu wakuu. Kujua kwamba hii ndiyo njia ya utakatifu kutakuwezesha kuweka kando tamaa ya kuhisi upendo wa Mungu na badala yake kumtamani Mungu Mwenyewe. Mungu si hisia; Yeye ni Utatu wa Nafsi za Kimungu. Jitahidi kumpenda bila kujali unavyohisi, na uhusiano wako Naye utakua na kufikia kina kikubwa kuliko unavyoweza kufikiri.
Bwana, nyakati fulani siuelewi upendo Wako mkamilifu kwangu. Ninapohisi kuwa karibu Nawe, ninashukuru sana kwa hali hii. Hata hivyo, nakuomba unipe neema ya kukupenda hata nisipohisi uwepo Wako. Tafadhali itakase imani yangu, Bwana mpendwa. Yesu, nakutumainia.
Tafakari ya 238: Uaminifu Nyakati za Giza
Ingawa Mtakatifu Faustina na watakatifu wengine wengi wakuu waliingia katika giza la kiroho la pekee, ambalo Mtakatifu Yohane wa Msalaba alilieleza kuwa “Usiku wa Giza wa Nafsi” na “Usiku wa Giza wa Roho,” sisi sote tutapitia “giza” fulani la namna moja au nyingine katika safari yetu ya imani. Huenda giza letu lisitokane na utakaso wa pekee wa nafsi unaotokea katika safari ya kuelekea ukamilifu, lakini mwitikio wetu lazima uwe uleule. Hata tupitie nini maishani, changamoto zinapotokea tunapaswa kusema maneno yaliyosemwa na watakatifu wakuu: “Mapenzi Yako yatimizwe!” Utakatifu unahusu kutenda Mapenzi ya Mungu licha ya mkanganyiko wowote au kile kinachoonekana kuwa kizuizi katika maisha yetu (Tazama Shajara #1237).
Tafakari juu ya kina cha usadikisho wako unaposali sala hii: “Mapenzi Yako yatimizwe!” Je, unamaanisha unachosema? Je, unaweza kusema hivyo kwa nguvu zote za akili, utashi na nafsi yako? Je, umechagua Mapenzi ya Mungu kuliko kila kitu kingine maishani? Kukubali Mapenzi ya Mungu wakati wa majaribu kunazaa matunda kwa namna ya pekee katika maisha ya imani. Vishawishi vinapokujia, hasa vishawishi vya kukata tamaa, unapaswa kuthibitisha upya azimio lako la kufuata Mapenzi makamilifu ya Mungu. Tafakari tendo hili takatifu leo. Sema maneno hayo na uyamaanishe kwa ukamilifu kadiri uwezavyo. Hakuna kitu maishani kinachopaswa kukuzuia kamwe kuifanya sala hii kuwa sala yako ya kila siku.
Bwana, Mapenzi Yako yatimizwe duniani kama huko Mbinguni! Ninaifanya hii kuwa sala yangu leo. Ninakutolea sala hii kwa tumaini kamili na kwa kujisalimisha Kwako kabisa. Ninakuchagua Wewe kuliko vitu vyote na kuyafanya Mapenzi Yako kuwa mapenzi yangu. Ninakupenda, Bwana wangu. Yesu, nakutumainia.
Tafakari ya 239: Muhuri wa Huruma
Kila mtakatifu mkuu ni kielelezo cha namna fulani ya wema wa Mungu. Baadhi huishi kwa kujitenga kwa namna ya pekee na tamaa ya mali za kidunia, wengine huwatumikia maskini kwa kujitoa bila kuyumba, wengine huishi maisha ya sala yenye kina, wengine hupokea mafunuo ya kifumbo, wengine huandika vitabu vingi vinavyofunua kina cha imani, lakini wote wameitwa kuidhihirisha Huruma ya Mungu kwa namna moja au nyingine. Huruma ya Mungu lazima iwe kama muhuri uliopigwa moyoni mwako. Huruma ya Mungu itaangaza kutoka katika maisha yako kwa namna ya pekee ambayo Yeye amekuchagulia. “Muhuri” wa Huruma ya Mungu utakuwa wa pekee, ukiangaza kama zawadi inayotolewa kupitia wewe tu. Uwe tayari kupokea namna ambazo Mungu amechagua kuangaza kutoka katika maisha yako. Ruhusu muhuri huo uangaze na kuonekana kwa wote, nawe utashuhudia mambo makuu yakitendwa na Mungu kupitia wewe (Tazama Shajara #1242).
Tafakari kuhusu moyo wako kutiwa muhuri wa kudumu na unaoonekana wa Huruma ya Mungu. Unatambua kwa namna gani kwamba Bwana anataka kuangaza Huruma Yake kupitia maisha yako? Ni kwa njia zipi halisi Huruma Yake iliyo Mbinguni inapaswa kushuka duniani kupitia wewe? Tafuta namna mahususi na halisi ambazo Huruma ya Mungu inadhihirishwa kupitia maisha yako. Kujitoa kwako kwa ajili ya kuidhihirisha Huruma Yake kwa namna hizi zinazoonekana na halisi kutakuwezesha kuwa chombo chenye nguvu cha Moyo Wake katika ulimwengu wetu.
Bwana, ninakupenda na ninatamani sana kukuruhusu udhihirishe Huruma Yako kupitia maisha yangu. Ninakuchagua Wewe kuwa chemchemi ya wema wote katika maisha yangu, nami ninakupa moyo wangu uutie muhuri wa huruma na upendo Wako. Angaza kupitia mimi, Bwana mpendwa. Yesu, nakutumainia.
Tafakari 240: Utamu au Uchungu Maishani?
Unapendelea lipi katika maisha yako? Kuhisi utamu au uchungu kila siku? Yaani, unatamani kufurahia mambo mengi ya maisha yako ya kila siku, au unatamani kwamba wajibu unaoutimiza kila siku ukuachie uchungu fulani katika hisi zako? Kwa watu wengi jibu ni rahisi. “Utamu” ni bora zaidi. Lakini je, ni kweli? Jambo la kuvutia ni kwamba kuhisi utamu au uchungu maishani si mwongozo mzuri wa kuelekea maisha ya utakatifu. Nyakati fulani, hata dhambi inaweza kuwa na ladha “tamu” kwetu, ilhali matendo ya utakatifu yanaweza kuwa na “uchungu” mwanzoni. Kuelewa jambo hili kutatuwezesha kuyakumbatia kwa kina zaidi Mapenzi ya Mungu. Lengo letu lazima liwe kutafuta Mapenzi Yake kwa ajili ya Mapenzi Yake pekee. Hatupaswi kupendelea furaha kuliko mateso yanayotokana na kuyakumbatia Mapenzi Yake, wala mateso kuliko furaha hiyo. Ikiwa Mapenzi ya Mungu yanadai sadaka kubwa, ikituachia hisia za mateso, basi na iwe hivyo. Ikiwa Mapenzi Yake yanatuvuta katika kupendana kunakotuachia furaha tamu, basi na iwe hivyo. Ingawa ni vigumu kufikia hali ya kutofungwa kabisa na mielekeo yetu, lazima tujitahidi kuifikia. Mapenzi Yake, na Mapenzi Yake pekee, lazima yawe kiini cha maisha yetu. Ni katika Mapenzi Yake pekee tunamogundua wingi wa Huruma Yake (Tazama Shajara #1245).
Tafakari tofauti kati ya Mapenzi ya Mungu na furaha au hali ya kutopendezwa unayoihisi unapoyakubali. Mapenzi Yake yanapokuita kujitoa sadaka, utapata hali hiyo kuwa ya aina fulani ya “uchungu.” Ni uchungu kwa maana kwamba huenda ikawa vigumu kwa hisia zako kuikubali. Usihangaike kuhusu jambo hili. Tafuta Mapenzi Yake katika mambo yote, na hatimaye furaha iliyo moyoni mwako itazidi hali nyingine zote unazopitia wakati huo. Mapenzi Yake yanafungua mlango wa Huruma Yake tele.
Bwana, ninatafuta Mapenzi Yako matakatifu sana katika mambo yote. Nisaidie kuyachagua Mapenzi Yako bila kujali ugumu wake au furaha yanayoleta. Unitakase, Bwana mpendwa, na unipe lengo moja tu maishani, ili kuyakumbatia kwangu yote unayoniita kufanya kuzae Huruma Yako kamilifu. Yesu, nakutumainia.
Tafakari 241: Tiba kwa Dhambi Zako Mahususi
Unazishindaje dhambi zako? Kila dhambi ni tofauti na inahitaji sala na sadaka mahususi ili kujinasua katika vifungo vyake. Aina tatu za dhambi zilizo za kawaida ni: dhambi za mwili, dhambi za hasira na dhambi za kiburi. Kila moja ya dhambi hizi inaweza kushindwa, lakini huenda ikahitaji uangalifu wa pekee. Ikiwa unapambana na dhambi za mwili, jaribu kufunga. Jinyime kile kinachokufurahisha kimwili kwa kuacha aina mbalimbali za vyakula au vinywaji wakati wa kufunga. Kwa dhambi za hasira, jaribu kumtendea jambo jema au kumwambia neno la fadhili mtu uliyemkasirikia. Mwombee na useme maneno ya Yesu Msalabani: “Baba, uwasamehe, hawajui wanachofanya.” Na kwa dhambi za kiburi, jaribu kusujudu kifudifudi mbele ya Bwana wetu kwa unyenyekevu wa sala, ukijivua yote mbele Yake. Jitahidi kutoa tiba hizi mahususi kwa ajili ya dhambi unazopambana nazo, na Huruma ya Mungu itamiminwa kwa wingi (Tazama Shajara #1248).
Ni dhambi zipi hasa unazopambana nazo? Hakikisha unafanya uchunguzi wa dhamiri kwa kina mara kwa mara, ukitafakari kwa undani kila moja ya Amri Kumi au dhambi kuu saba. Ukishazitambua dhambi kuu unazopambana nazo, hasa zile ulizozoea kuzifanya, tafuta tiba takatifu kwa ajili yake. Matendo ya kitubio kwa ajili ya dhambi ni kama dawa. Unahitaji dawa inayofaa kwa kila ugonjwa. Uwe tayari kupokea njia ambazo Mungu anakufunulia “dawa” hizi kwa ajili ya roho yako, na uzitumie bila kusita. Kila tendo la kitubio unalofanya litafungua mlango wa Huruma katika maisha yako kwa namna mpya na ya kina.
Bwana, ninajua kwamba mimi ni mgonjwa kwa sababu ya dhambi zangu nyingi. Mimi ni dhaifu na ninahitaji kuponywa. Nisaidie kuziona dhambi zangu na kuzikabili kwa Huruma Yako. Unipe njia za kuzishinda ili niweze kukukaribia zaidi. Ninakupenda, Bwana; uniweke huru kutoka kwa yote yanayonitenga na Wewe. Yesu, nakutumainia.
Tafakari 242: Uzuri wa Kweli Unaong’aa kwa Namna ya Pekee
Imesemwa kwamba “uzuri” hutegemea macho ya mtazamaji. Yaani, wengine husema kwamba maana ya uzuri hutegemea upendeleo binafsi wa mtu mmoja au mwingine. Ingawa huenda jambo hili likawa na ukweli fulani kwa mtazamo wa juu juu, kwa undani zaidi uzuri wa kweli hutoka kwa Mungu na ni halisi katika kila hali, bila kutegemea maoni ya mtu. Hautegemei upendeleo wetu binafsi; badala yake, unamtegemea Mungu. Kadiri kitu au mtu anavyofanana zaidi na Mungu na Huruma Yake, ndivyo uzuri wake unavyoongezeka. Ni muhimu kujua hili kuhusu roho zetu. Sote tunataka wengine watuone kuwa “wazuri.” Lakini lazima pia tuelewe kwamba hili linawezekana tu kwa kuishi maisha ya utakatifu. Na jambo la ajabu ni kwamba uzuri wa kila mtu ni wa pekee. Mbinguni, hatutakuwa sote sawa; badala yake, upekee wa kila mtu utaangaza mng’ao wa Mungu kwa namna ya pekee, inayomhusu mtu huyo tu. Jitahidi kuruhusu uzuri na fahari ya Mungu viangaze kupitia maisha yako ili uwe chombo cha utukufu Wake (Tazama Shajara #1251).
Je, unatamani kuwa mzuri? Huenda hili ni swali ambalo wanawake wanaweza kulijibu kwa urahisi zaidi kuliko wanaume, kwa kuwa neno hili hutumiwa zaidi kuwahusu wanawake. Lakini litafakari swali hili. Unapofanya hivyo, jaribu kuutazama uzuri kwa mtazamo tofauti. Katika maana yake ya ndani kabisa, uzuri si mvuto wa asili wa mwili. Uzuri wa kweli ni kushiriki katika utukufu wa Mungu na kuuruhusu utukufu huo uangaze kupitia roho yako kama vile nuru inavyopita katika mche wa kioo. Jitahidi kumruhusu Mungu aangaze kupitia kwako ili uzuri wa Mungu uwabariki wengine kwa Huruma Yake kwa namna ya pekee na ya kina.
Bwana, Wewe ndiwe utukufu na fahari ya roho yangu. Uzuri Wako unatia kicho na unang’aa katika kila hali. Njoo uishi ndani yangu na uangaze kupitia mimi ili wengine wauone uzuri Wako unaobadilisha maisha yangu. Ninajitoa Kwako, Bwana mpendwa, kuwa chombo cha utukufu Wako. Yesu, nakutumainia.
Tafakari 243: Zawadi ya Pekee ya Yesu kwa Wale Anaowapenda
Ungemtendeaje mtu unayempenda? Kwa kawaida, kwa wanafamilia au marafiki wa karibu sana, tunawatakia yaliyo bora kwao na yanayowaletea furaha. Mungu anamtakia kila mmoja wetu vivyo hivyo, lakini tunaweza kushangazwa na kile ambacho Mungu anakiona kuwa chanzo cha furaha yetu na anachokiona kuwa bora kwetu. Zaidi ya hayo, ingawa upendo wa Mungu ni mkamilifu kwa kila nafsi, ni sahihi pia kusema kwamba upendo wa Mungu huwa wa kina zaidi kwa wale wanaomkaribia. Si kwamba upendo Wake unabadilika, bali kwamba upendo Wake unapokewa na kuonwa kwa kina zaidi. Hilo linapotokea, Mungu anaweza kuudhihirisha upendo Wake kwa namna ya kina sana. Na upendo wa Mungu unapopokewa na nafsi kwa kina cha ndani kabisa, mara nyingi huwa ni upendo unaoiita nafsi hiyo kuingia katika mateso. Ikiwa hilo linakushangaza, fikiria tu upendo mkamilifu wa Baba kwa Yesu. Baba, katika upendo Wake mkamilifu kwa Mwana, alimwita kwenda Msalabani. Lakini katika Msalaba huo, nafsi ya kibinadamu ya Yesu iliweza kuudhihirisha upendo wa Baba kwa namna ya kina kabisa. Hili ni fumbo gumu kuelewa, hivyo usiwe na wasiwasi ikiwa ni vigumu kulielewa mara moja. Jua tu kwamba mara nyingi Mungu huruhusu mateso makubwa ya kiroho katika maisha ya wale ambao wamevutwa kuingia katika uhusiano wa ndani sana Naye (Tazama Shajara #1253).
Tafakari upendo mkamilifu wa Baba anayemwita Mwanawe kwenda Msalabani. Tulia ukilitafakari hilo na ujitahidi kupenya maana yake. Ukiweza kuelewa jinsi upendo wa Baba ulivyoweza kumwita Mwana atoe sadaka hii, basi utaanza kuelewa upendo mkamilifu wa Mungu kwako anapokuita kuishi maisha ya kujitoa sadaka. Usidhani kwamba upendo wa Mungu utafanya maisha yako yawe “rahisi.” Upendo Wake utayafanya maisha yako yawe yenye utukufu, lakini kuna uwezekano mkubwa kwamba hilo litatimia kupitia mateso.
Baba, fumbo la mateso ya Yesu, Mwana Wako, linazidi ufahamu wangu. Nisaidie kuyaelewa kwa ukamilifu zaidi mapenzi Yako ya fumbo na kutambua kwamba mateso katika maisha haya mara nyingi ni ishara ya upendo Wako. Katika mambo yote, yaweke macho yangu kwenye Msalaba, Bwana mpendwa. Yesu, nakutumainia.
Tafakari 244: Kufanya Kazi Hadi Mwisho wa Dunia
Ikiwa unajitahidi, mchana na usiku, kueneza kazi za Mungu, hilo ni jambo jema. Matunda mema yatatokana na kujitoa kwako kutimiza mapenzi ya Mungu na kueneza Huruma Yake ya Kimungu. Lakini tunapaswa pia kutambua kwamba Mungu anaweza kututumia kueneza Huruma Yake hadi mwisho wa dunia. Kwa namna gani? Mungu pekee ndiye anayejua. Lakini kwa hakika anatamani kukutumia kwa kusudi hili. Baadhi ya watu, kama Mtakatifu Faustina, walitumiwa kuanzisha ibada ya Huruma ya Mungu, na ibada hiyo itaendelea hadi Yesu atakaporudi. Wengine, na huenda wengi wetu, wameitwa kuchangia kazi ya kudumu ya Huruma kwa njia nyingine mbalimbali. Kwa mfano, tendo moja la upendo litaleta jambo jema katika maisha ya mtu mwingine, ambalo linaweza kumbadilisha kwa namna itakayoanzisha kazi ya Huruma ya milele. Au fikiria sala yako kwa ajili ya wale waliokabidhiwa wajibu maalumu, kama vile kusali kwa ajili ya Papa, maaskofu au mapadre. Au fikiria ukweli kwamba utakatifu wako unaoupata hapa na sasa utaongezeka Mbinguni na kukuwezesha kuliombea Kanisa daima. Uwe na bidii sasa katika kazi yako ya kueneza Huruma ya Mungu, lakini pia tambua kwamba kazi hii lazima iendelee hata milele. Lizingatie hili kama lengo lako, na Mungu atatumia juhudi zako za sasa kwa njia zisizowazika katika nyakati zote (Tazama Shajara #1256).
Unapofikiria kazi ambayo Mungu amekukabidhi, je, unaiona kama jambo linaloweza kuwa na matokeo ya milele? Je, unajiona kama “kiungo katika mnyororo” ambacho Mungu anatamani kukitumia kuliimarisha Kanisa katika nyakati zote? Uwe tayari kulipokea lengo hili na umruhusu Bwana akutumie kwa njia ambazo usingeweza kamwe kuziwazia mwenyewe.
Bwana, maisha yangu ni Yako. Ninajitoa Kwako kwa kusudi la kueneza Huruma Yako sasa na milele. Unitumie upendavyo, Bwana mpendwa. Ninajitoa kuwa chombo kilicho tayari kutumikia Huruma Yako katika ulimwengu wetu. Yesu, nakutumainia.
Tafakari 245: Ukali Ulioahirishwa
Ni muhimu kujua kwamba Yesu ana haki kamili ya kutekeleza haki Yake hapa na sasa. Ana haki kamili ya kututendea kwa ukali kwa sababu ya dhambi zetu na kututolea hukumu ya milele. Ukweli huu mara nyingi husahaulika kwa sababu ya Huruma Yake. Lakini hatupaswi kamwe kuusahau ukweli huu. Ni muhimu kukumbuka hili kwa sababu tusipoelewa haki kamili aliyo nayo Mungu ya kuutekelezea ulimwengu hukumu ya haraka na isiyoweza kubatilishwa, hatutaelewa kamwe kwamba kujizuia Kwake ni tendo la Huruma isiyo na kipimo. Mama wa Mungu amekabidhiwa kwa namna ya pekee jukumu la kuomba Huruma Yake na kusihi kwa niaba yetu ili ghadhabu ya Mwanawe izuiwe. Mungu alimpa jukumu hili la kutuombea, Naye anazisikiliza sala hizo. Pia anamwita kila mmoja wetu kuomba Huruma kwa ulimwengu na, ingawa sala zetu hazina nguvu kama zile za Mama wa Mungu, zinaweza kuwa na nguvu hizo tukiziweka katika Moyo wake Safi usio na doa. Kumkabidhi Mama yetu Mbarikiwa sala zetu huongeza nguvu zake na kuzigeuza kuwa chombo cha neema isiyopimika, kikizuia mkono wa Haki ya Mungu (Tazama Shajara #1261).
Je, unaielewa haki aliyo nayo Mungu ya kukutolea hukumu ya ghafla na kali? Huenda si jambo la kufurahisha kulifikiria, lakini ni muhimu kulielewa. Tafakari ukweli huu leo. Uuamini na ujue kwamba anazuia hukumu Yake kwa sababu ya Huruma Yake. Omba leo maombezi ya Mama yetu Mbarikiwa, na umkabidhi sala zako mwenyewe. Kwa njia ya sala zako, zinazotolewa kwa maombezi yake, haki ya Mungu inazuiwa na Huruma Yake itajaliwa katika wakati wetu.
Mama mpendwa sana, leo ninakutolea sala zangu zote, kazi zangu na sadaka zangu ili nawe umtolee Mwana wako. Tafadhali uniombee mimi na watoto wako wote ili haki ya Mwana wako izuiwe huku Huruma Yake ikimiminwa. Yesu, nakutumainia.
Tafakari 246: Baada ya Kupokea Komunyo Takatifu
Unafanya nini baada ya kupokea Komunyo Takatifu? Je, unarudi kwenye kiti chako kanisani huku ukiwa umetatizika mawazo, akili yako ikitangatanga, ukiwaangalia wengine walio karibu nawe, na kushindwa kukutana na Bwana wetu kwa namna ya kweli ya kiroho? Au unaruhusu wakati huo uwe wakati wa sala ya kweli na ushirika na Mungu? Ikiwa kwa kweli unafanya hayo ya kwanza, uwe tu mkweli kwako mwenyewe na kwa Mungu, na utumie utambuzi huo kama fursa ya kuchunguza upya jinsi unavyoikaribia Karama hii takatifu kabisa! Wakati unaofuata baada ya Komunyo Takatifu ni wakati wa thamani ambamo kila nafsi inaalikwa kutwaliwa kabisa na Yeye ambaye imempokea muda huo kama chakula. Kwa maneno mengine, kupokea Komunyo Takatifu si tendo la kimwili tu tunalofanya; lazima pia liwe jambo ambalo Mungu anatufanyia. Lazima tuchague si tu kumla Bwana wetu, bali pia kumruhusu atutwae kabisa kwa Huruma Yake. Hakuna wakati bora wa kufanya hivyo kuliko muda unaofuata baada ya kupokea Karama hii yenye thamani isiyopimika. Hili linatimizwa kwa kuyafanya maisha yako kuwa sadaka kwa Mungu. “Sadaka” ni kitu kinachotolewa, na kupokea Komunyo Takatifu lazima kuwe wakati ambamo tunajitoa kabisa kwa Bwana wetu aliye Mungu (Tazama Shajara #1264).
Tafakari kuhusu mara ya mwisho ulipopokea Komunyo Takatifu. Je, ulipata uzoefu wa namna gani? Je, ulikuwa umeelekeza mawazo yako yote katika kile ulichokuwa ukifanya? Je, ulijitoa kwa Bwana wetu kama sadaka ya upendo? Je, ulijiweka mikononi mwa Bwana wetu kwa moyo wa kujitolea sadaka? Je, ulimruhusu Bwana wetu akugubike kwa upendo Wake wenye huruma? Yatafakari maswali haya na ujitoe kwa dhati kufikia kina hiki cha kujitolea. Ukifanya hivyo, Komunyo Takatifu itakuwa tendo kuu kuliko yote la Huruma katika maisha yako.
Bwana wangu na Mungu wangu, ninajitoa Kwako kwa kujikabidhi na kujisalimisha kabisa. Maisha yangu ni Yako, Bwana mpendwa. Ninajitoa Kwako bila kubakiza chochote, kama sadaka ya upendo. Yesu, nakutumainia.
Tafakari ya 247: Baraka ya Watu Wenye Mahitaji
Ikiwa mtu katika familia yako angekuwa mgonjwa sana, au gerezani, au katika hali fulani ya uhitaji mkubwa, je, hilo lingekuwa mzigo kwako au baraka? Litafakari hilo. Je, watu wenye mahitaji maalumu wanafanya maisha yako yawe magumu zaidi? Ikiwa swali hili lingejibiwa kwa kuangalia mambo ya kila siku tu, jibu lingeweza kuwa, “Ndiyo.” Lakini likijibiwa kwa mtazamo wa ndani zaidi wa kiroho, jibu ni kwamba wale “wanaotubebesha mzigo” kwa mahitaji yao mahususi wanatupatia fursa ya kufikia utakatifu mkuu. Hivyo ndivyo ilivyo kwa sababu watu wenye mahitaji maalumu wanatuhimiza kuitikia kwa mapendo, huruma na huduma ya Huruma. Tukiwaona kama mzigo, tunakosa fursa ya pekee ya kupata neema. Mara nyingi Mungu huwaruhusu wengine wateseke na kutubebesha mzigo mtakatifu ili kutuwezesha kuidhihirisha Huruma Yake. Watafute watu hawa wa pekee na uwapatie upendo, utunzaji na Huruma iliyomo katika Moyo wa Yesu (Tazama Shajara #1268).
Mungu amemweka nani katika maisha yako? Hasa, ni nani anayebeba mateso, ugonjwa, udhaifu au shida ya pekee inayohitaji umtunze kwa uangalifu zaidi? Anaweza kuwa mtoto mgonjwa, mwenzi wa ndoa mwenye huzuni kubwa, mzazi mzee, mtu ambaye dhambi zake ziko wazi au rafiki mwenye uhitaji. Yeyote anayekujia akilini, jitahidi kumwona yeye na mahitaji yake kama mwaliko uliojaa neema kutoka kwa Bwana wetu, wa kudhihirisha upendo na Huruma Yake. Yeye ni baraka kubwa kwako kuliko utakavyoweza kutambua. Ruhusu mahitaji yake yaamshe huruma na utunzaji vilivyo katika Moyo wa Kristo ili vidhihirike kupitia kwako.
Bwana, tafadhali unipe moyo unaofanana na Wako. Unipe Moyo Wako mkamilifu wenye Huruma na rehema ili niweze kuudhihirisha upendo Wako mkamilifu kwa wengine. Nisaidie kuwaona watu wote kama zawadi na kutambua hadhi yao isiyo na kikomo. Nami ninapojitahidi kuwapenda, ninakushukuru kwa baraka ninazopokea katika tendo hili lisilo na ubinafsi. Yesu, nakutumainia.
Tafakari ya 248: Rasilimali Zisizo na Kikomo
Hebu fikiria kama ungepata chanzo cha rasilimali za asili zisizo na kikomo kwa kutengeneza mashine inayobadili kiasi kidogo tu cha oksijeni kuwa kiasi kisicho na kikomo cha nishati. Ungehitaji tu kuiwasha mashine uliyotengeneza, nayo ingezalisha nishati bila mwisho. Huo ungekuwa uvumbuzi wa ajabu sana. Lakini kitu kama hicho kipo katika maisha ya kiroho. “Oksijeni” inayoiendesha ni unyonge na dhambi zetu. Na “jenereta” ni Moyo wa Yesu. “Nishati” inayozalishwa ni Huruma ya Mungu isiyo na mwisho. Laiti tungeweza kuelewa hili, ulimwengu wetu ungefurika rasilimali hii ipitayo maumbile kwa kiasi kisicho na kikomo. Lazima tutambue kwamba Mungu hubadili unyonge wetu katika maisha tunapomtolea. Kwa kweli, hii ndiyo shauku Yake inayowaka. Moyo Wake unatamani kuubadili unyonge wako kuwa Huruma Yake ili maisha yako mwenyewe yajazwe kwa wingi, na ili, kupitia kwako, ulimwengu ujazwe kwa wingi. Mpe Mungu unyonge na dhambi zako, na umruhusu aendelee kuvibadili bila mwisho (Tazama Shajara #1273).
Una maoni gani kuhusu unyonge na dhambi zako mwenyewe? Je, unavificha, unavifunika, unavipuuza na kujifanya kwamba havipo? Je, unaishi ukiwafanya wengine waone kana kwamba una maisha yasiyo na dhambi wala unyonge? Baadhi ya watu hufanya hivyo, na wengine hupita kiasi upande wa pili, wakijitumbukiza katika kujihurumia na kuonyesha unyonge wao ili wote wauone kana kwamba unyonge huo ni alama ya heshima. Hakuna njia yoyote kati ya hizo inayosaidia. Njia pekee inayosaidia ni kukabidhi dhambi zako na unyonge wako wote kwa Moyo wa Yesu. Unaweza kufanya hivyo. Unahitaji tu kuchagua kufanya hivyo. Fanya hivyo leo. Anza kufanya tendo hili la kujisalimisha kabisa, nawe utagundua nguvu ya kimiujiza iliyomo katika Moyo wa Yesu ya kubadili kila kitu kuwa Huruma.
Ee Moyo wa Yesu, ninakimbilia Kwako nikiwa na unyonge na maumivu yangu, nami ninakabidhi dhambi zangu Kwako, Bwana mpendwa. Tafadhali uvibadili kuwa Huruma Yako, ukiwezesha zawadi hii kuwa chanzo cha neema isiyo na mwisho. Yesu, nakutumainia.
Tafakari ya 249: Tunda la Mateso
Ni baada tu ya mtu kuteseka sana ndipo anapoanza kuelewa matunda mema yanayoweza kutokana na mateso hayo. Yenyewe, mateso ni matokeo ya hali yetu ya kibinadamu iliyoanguka katika dhambi. Lakini kwa kuwa Yesu aliingia katika hali yetu ya kibinadamu, akayakubali mateso yote na kuyakomboa, sasa mateso yana nguvu kubwa tunapoyakubali kwa hiari na kuyaunganisha na mateso ya Yesu. Tunda moja jema linaloweza kutokana na mateso ni ujuzi wa kiroho. Tunapoyakubali mateso katika Kristo na kuyatolea Kwake kama sadaka iliyounganishwa na Sadaka Yake mwenyewe, tutatambua kwamba mateso yetu yanatusaidia kuyaelewa maisha kwa uwazi, kuyaona katika mtazamo unaofaa, na huenda hata yakatupatia kipawa cha kiroho cha kutambua hali ya nafsi za watu wengine tunaokutana nao. Kipawa hiki cha kuzijua nafsi za wengine kitatuwezesha kuona mahitaji yao na kuwapatia Huruma ya Mungu kwa namna mahususi wanayoihitaji. Usiogope kuruhusu mateso yako yakubadilishe na kukupatia kipawa hiki cha ujuzi pamoja na vipawa vingine vingi ambavyo Mungu anataka kukujalia (Tazama Shajara #1277).
Tafakari jinsi unavyokabiliana na mateso yako mwenyewe. Iwe ni adha ndogo unayoihisi au maumivu makali ya ndani, kila tunachopitia maishani kinaweza kukombolewa na kubadilishwa ili kitubadilishe sisi. Ikiwa unaamini hili, basi jitahidi kuyakubali kwa makusudi maudhi yote na mateso yote unayovumilia kama sadaka kwa Mungu. Mtolee hayo, kisha ruhusu utakaso unaotokana na kuyakubali huko kwa hiari uzae matunda mema kwa wingi katika maisha yako.
Bwana, mara nyingi sana ninayakimbia mateso yangu na kukataa matokeo ya ukombozi ambayo kuyakubali mateso yangu kwa hiari kunaweza kuleta ndani yangu. Nipe ujasiri wa kusema “Ndiyo” kwa misalaba ninayopewa na kuwa tayari kupokea matunda ya kiroho ambayo inaweza kuzaa katika maisha yangu. Nakupa yote, Bwana mpendwa. Yesu, nakutumainia.
Tafakari 250: Kusali Ukiwa Umesujudu Kifudifudi Hadi Chini
Unaposali, unamwendeaje Bwana wetu? Hakika ni jambo jema kumtolea siku yako yote kwa ibada yenye upendo na kuzungumza Naye siku nzima kama unavyozungumza na rafiki yako wa karibu zaidi. Lakini kuna nyakati nyingine ambapo sala yetu lazima iwe ya dhati sana na inapaswa kuonyeshwa kwa namna yenye kudhihirisha udhati huo. Njia moja ya kufanya hivyo ni kusujudu kwa mwili kabisa kifudifudi mbele ya Bwana wetu. Katika ukimya wa chumba chako au kanisani pasipo na watu, tafuta fursa ya kusali kwa namna hiyo. “Udhati” huo lazima uwe wa kujisalimisha kikamilifu kwa Bwana wetu. Lazima udumu kwa muda mrefu na uambatane na kujivua nafsi. Kusali kwa namna hiyo ni tendo zuri la upendo na ni njia ya kumwabudu Mungu kama anavyostahili. Ingawa hatuwezi kamwe kumwabudu kikamilifu, jitihada zetu za kufanya hivyo kwa ukamilifu kadiri tuwezavyo zinampendeza na kumwezesha kutusogeza karibu na Moyo Wake uliojaa Huruma tele (Tazama Shajara #1279).
Je, umewahi kusali ukiwa umesujudu kifudifudi mbele ya Bwana wetu? Ikiwa umewahi kufanya hivyo, endelea. Tafuta fursa ya kufanya hivyo kila siku. Ikiwa hujawahi, basi huu ni wakati mzuri wa kuanza. Usiwe na wasiwasi kuhusu utakachosema wala usiwe na wasiwasi ikiwa mwanzoni utahisi kutokuwa na raha. Piga tu magoti, uiname hadi chini, na uonyeshe upendo wako kwa Bwana wetu. Kaa hapo na ujaribu kufanya tendo la kujisalimisha kabisa. Bwana atapokea tendo lako la kuabudu na kukuvuta karibu zaidi na Moyo Wake Mtakatifu wenye Huruma.
Bwana, ninasujudu kifudifudi mbele Yako na kukutolea maisha yangu yote kama zawadi isiyo na ubinafsi kwa ajili ya utukufu Wako. Nakupa yote, Bwana mpendwa, nami ninaomba nisibakishe chochote. Wewe ndiwe Mungu wangu na yote kwangu. Ninakupenda na kuyasalimisha maisha yangu Kwako. Yesu, nakutumainia.
Tafakari 251: Makao ya Ndani ya Moyo Wako
Bwana anatamani kuja kwako na kufanya makao Yake ndani ya moyo wako. Lakini anapokuja kwako, anakuta nini? Moyo wako uko katika hali gani? Baadhi ya mioyo ni kama bustani ya waridi yenye harufu nzuri. Kuna nuru, uzuri, fahari na mng’ao. Ni mahali pa kupumzika kwa amani na mahali palipotakaswa kwa uwepo wa Bwana wetu. Mioyo mingine ni kama chumba cha gereza chenye giza, baridi, upweke na huzuni. Hizi ni nafsi zilizonaswa katika mzunguko wa dhambi na ambazo zimeshindwa, tena na tena, kumruhusu Bwana aingie. Lakini kwa hakika anachagua kuingia moyoni mwako, bila kujali hali yake. Uwe ni uwanja wa waridi wenye harufu nzuri au giza na upweke wa gereza, Bwana anataka kuingia (Tazama Shajara #1280).
Tafakari chumba cha ndani cha moyo wako. Makao haya yakoje? Uwe mkweli na umfunulie Bwana wetu mahali hapa pa siri. Ikiwa moyo wako unafanana zaidi na gereza la chini ya ardhi lenye ukiwa, baridi, giza na upweke, basi ujue kwamba wewe, kuliko mtu mwingine yeyote, unaalikwa kupokea Huruma ya Mungu. Anatamani kuja kwako na kufungua mlango wa gereza hilo ambamo unahisi umenaswa na kutengwa. Hakuepuki katika giza hili, naye ataingia ndani. Lakini anapoingia, anafanya hivyo ili akuweke huru. Anatamani kuigeuza nafsi yako iwe mahali pa furaha tamu. Hili linahitaji juhudi, kujisalimisha, ukweli, unyenyekevu na matumaini. Lakini Mungu anaweza kufanya yote na anaweza kuigeuza hata nafsi iliyo katika hali mbaya kuliko zote iwe bustani ya uzuri na upendo. Huruma Yake hutoa udongo, Jua, mbegu, maji na kila kitu kinachohitajika ili kuumba upya chumba cha ndani cha nafsi yako. Tafakari ukweli huu na uanze mabadiliko yako leo.
Bwana wa thamani, nakupa chumba cha ndani cha nafsi yangu. Njoo upumzike ndani yangu, ukiubadilisha moyo wangu uwe makao Yako matakatifu. Nakupa, Bwana mpendwa, yote niliyo na yote niliyo nayo. Niumbe upya na kunifanya mpya. Yesu, nakutumainia.
Tafakari 252: Utume wa Huruma na Kukubali
Baadhi ya watu wanahangaika sana maishani na wanaonekana kushindwa kutatua matatizo yao. Wao ni “wenye uhitaji” kwa maana kwamba daima wanatafuta kitu cha kuwapa faraja. Huenda wakaamini kwamba wanachotaka ni utajiri au aina nyingine za faraja za kidunia, lakini wasichotambua ni kwamba Bwana ndiye jibu la mahitaji yao yote. Nafsi hizi zinazotangatanga zinapaswa kuwa walengwa wakuu wa huruma yetu. Njia moja ya kuwafikishia Huruma ya Mungu ni kuwa karibu nao kwa upole, tukiwa na moyo unaowakubali na sikio la kuwasikiliza. Wale waliolemewa na mizigo mizito ya maisha wanapogundua kwamba tunawajali na tunataka kuwasikiliza, mara nyingi watatumia fursa hiyo kutufungulia mioyo yao, wakitufunulia majeraha na mahangaiko yao. Si kwamba jukumu letu hasa ni kuwaponya au kutatua matatizo yao. Mara nyingi jukumu letu ni kuwajulisha tu kwamba tunawajali na tunawaelewa. Tendo hili la upendo na kuwakubali wengine ni tendo la Huruma ya pekee inayotiririka kutoka katika Moyo wa Yesu kupitia kwetu (Tazama Shajara #1282).
Unapokutana na watu wenye mahangaiko na wanaolemewa na mizigo mizito maishani, unawatendeaje? Je, unawahukumu na kuwachukia? Au unawasikiliza, unajitahidi kuwaelewa, na kuwapokea kwa moyo wenye huruma? Tafakari swali hili na uwafikirie wale ambao Mungu amewaweka katika maisha yako, wanaohitaji kujua kupitia kwako kwamba Mungu anawapenda na kuwapokea. Usipuuze tendo hili, kwa maana umeitwa kuwa mtume wa Huruma ya Mungu.
Bwana, ninajitoa Kwako kuwa mtume wa Moyo Wako wenye huruma. Nijalie huruma ya kweli na moyo wa kuzikubali nafsi zinazohitaji zaidi Huruma Yako ya Kimungu. Nisaidie kuwasikiliza, kujitahidi kuwaelewa na kuwa karibu nao kama mwakilishi wa Moyo Wako Mtakatifu. Ninajitoa Kwako, Bwana mpendwa. Unitumie utakavyo. Yesu, nakutumainia.
Tafakari 253: Mwitikio wa Shukrani Kamili
Mwitikio wetu kwa Mungu unapaswa kuwa upi? Mara nyingi tunajishughulisha kupita kiasi na nafsi zetu wenyewe katika uhusiano wetu na Mungu. Tunakazia fikira mahangaiko na mahitaji yetu. Tunapaswa kuyakabidhi kwa Mungu na kuyaachilia. Tunapofanya hivyo, tutagundua kwamba tunaanza kuona utukufu na wema wa Mungu ukitenda kazi maishani mwetu, nasi tutaanza kujawa na shukrani kuu kwa Mungu. Shukrani zinapaswa kututawala na kuzijaza fikira na sala zetu. Tunapaswa kuruhusu shukrani zitawale misukumo na hisia zetu na kila sehemu ya utu wetu. Hilo ndilo tutakalofanya milele. Maisha ya mbinguni yatakuwa tendo moja la milele la kumshukuru Mungu kwa wema na Huruma Yake. Tunapoweza kuacha kujitazama wenyewe na kumkazia Mungu macho, zawadi hii ya shukrani itaanza kuongoza maisha yetu (Tazama Shajara #1285-1286).
Je, una moyo wa shukrani? Utakuwa na moyo wa shukrani ikiwa tu utajiruhusu kuona zawadi zisizohesabika ambazo Mungu anakumiminia kila siku. Ni rahisi kuruhusu kujishughulisha na sisi wenyewe tu kutufumbe macho tusizione baraka hizi zisizohesabika kutoka kwa Mungu. Lakini ukiweza kuelekeza macho yako Mbinguni na kuona ukweli, utastaajabia wema wa Mungu usio na kikomo. Usijikoseshe furaha ya kugundua yote ambayo Mungu anakutendea mchana na usiku. Usifumbie macho wingi wa Huruma Yake. Tafakari leo ikiwa unajiruhusu kuuona upendo Wake wenye huruma anaokumiminia wewe na wengine. Kaza macho yako kwenye Huruma hii na uruhusu utambuzi huu ukuze ndani yako moyo wenye shukrani za dhati.
Bwana wangu, ninakushukuru kwa yote uliyotenda maishani mwangu, na ninakushukuru kwa yote utakayoendelea kutenda ndani yangu. Nisaidie nizidi kuutambua upendo Wako wenye huruma na baraka zisizohesabika unazonijalia mimi na watoto Wako wote. Ninapoziona kazi za mikono Yako kila upande, ujaze moyo wangu shukrani za dhati. Yesu, nakutumainia.
Tafakari 254: Kushirikishwa katika Uungu
Wito wetu maishani unaweza kuelezwa kama wito wa kushirikishwa katika uungu. Hii ina maana gani? Ina maana kwamba Mungu alikuja duniani na kutwaa asili yetu ya kibinadamu ili atuvute tushiriki katika uzima Wake mwenyewe. Kwa maana fulani, tumeitwa kuwa Mungu. Wazo hili la “kushirikishwa katika uungu” lilikuwa la kawaida miongoni mwa Mababa wa Kanisa la mwanzo kama vile Ireneo, Yustino Shahidi, Atanasio, Klementi wa Aleksandria na Mtakatifu Augustino. Si kwamba tunapaswa kuwa Mungu kwa maana ya asili yetu kuwa ya kimungu; hilo lingekuwa uzushi. Badala yake, tumeitwa kuwa Mungu kwa maana ya kushiriki katika uzima Wake wa kimungu, tukiwa kitu kimoja Naye katika muungano mkamilifu. Ni kana kwamba Mungu angekuwa Bahari nasi tungekuwa tone la maji lililotumbukizwa katika Bahari hiyo. Ingawa chembe hususa za tone la maji linalotuwakilisha zinabaki kuwa tone hilo moja, tone hilo linafyonzwa na maji ya Bahari inayomwakilisha Mungu. Muungano wetu Naye unapaswa kuwa kamili kiasi kwamba Mungu anaishi ndani yetu nasi tunaishi ndani ya Mungu (Tazama Shajara #1289).
Tafakari juu ya wito wako wa kufanywa mshiriki wa uzima wa Mungu. Dhana hii inagusa kiini cha wito wetu wa Kikristo kwa kuwa inaeleza muungano wa kina ambao tumeitwa kuwa nao na Mungu wetu mwenye huruma. Anataka ushiriki uzima Wake na kuwa kitu kimoja Naye kwa kila namna. Ingawa huenda ikawa vigumu kuelewa jambo hili, unapaswa kulikubali kwa imani kuwa ndilo wito wako. Tafakari juu ya dhana hii leo na umwambie Bwana wetu kwamba unajitoa Kwake ili uwe kitu kimoja Naye na kushiriki uzima Wake mwenyewe.
Bwana, tafadhali njoo kwangu na unishirikishe katika uungu kulingana na Mapenzi Yako makamilifu na Huruma Yako tele. Ninakushukuru kwa kuniita katika wito wenye utukufu na ulio mkuu namna hii maishani, nami ninaukubali mwaliko huu kutoka Kwako. Maisha yangu ni Yako, Bwana mpendwa; unibadilishe, unitawale kabisa, na unitendee utakavyo. Yesu, nakutumainia.
Tafakari 255: “Baraka” ya Dhambi
Huenda kichwa hiki kikaonekana kuwa kisicho cha kawaida. Dhambi inawezaje kuwa “baraka?” Ni kweli kwamba, kwa maana halisi, dhambi ni kosa dhidi ya Mungu na ina athari ya kututenga na Mungu. Hivyo, dhambi si baraka kwa maana halisi. Lakini Mungu ni Mwenyezi na anaweza kutumia kila kitu kwa utukufu Wake, hata dhambi yetu. Dhambi inaweza kuitwa baraka kwa maana hii tu: tunapoziona dhambi zetu, kuzikiri, kujinyenyekeza mbele ya Mungu na kuomba kwa unyenyekevu Huruma Yake, Yeye hutujalia huruma hiyo kwa wingi usio na kipimo. Mwishowe, matokeo ya unyenyekevu wa toba huleta mema makubwa zaidi kuliko madhara yaliyosababishwa na dhambi. Mungu anaweza kurekebisha madhara hayo mara moja, na anapofanya hivyo, anatupatia Huruma ambayo si tu inatuponya, bali pia inatuinua na kutusogeza karibu zaidi na Moyo Wake. Ruhusu dhambi yako igeuzwe kuwa baraka kwa nguvu ya Mungu, nawe utastaajabia Huruma Yake isiyo na mwisho (Tazama Shajara #1293).
Tafakari mtazamo ulio nao kuhusu dhambi yako. Mara nyingi sana unaweza kuikana dhambi yako, kuitetea au kuifumbia macho. Hili ni kosa kubwa kwa sababu mbili. Kwanza, kufanya hivyo kunakuzuia kutubu. Pili, kutotubu kwa unyenyekevu kunakuacha bila huruma tele ya Mungu. Sitawisha moyoni mwako hamu kubwa ya kuona kila dhambi unayotenda. Jitahidi kutambua kila dhambi, hata mapungufu madogo kabisa. Kuzingatia hata mapungufu yako ya kiroho kutakuwezesha kujinyenyekeza mbele ya Mungu kwa namna ambayo unyoofu wako na kujichunguza kwako kwa makini vitaleta baraka zisizohesabika maishani mwako.
Bwana Yesu, Mwana wa Mungu, unihurumie mimi mwenye dhambi. Bwana, ninaiona dhambi yangu, lakini pia ninatambua kwamba siioni kwa uwazi wa kutosha. Tafadhali unijalie neema ya kuona kila dhambi yangu, hata upungufu mdogo kabisa, kisha unijalie neema ya kutubu kwa unyenyekevu, kwa moyo mnyoofu na wenye majuto. Ninatumainia wingi wa huruma Yako, Bwana mpendwa. Yesu, nakutumainia.
Tafakari 256: Kufanya Kadiri ya Uwezo Wako Wote
Mtakatifu Mama Teresa hunukuliwa mara nyingi akisema kwamba Mungu anatutaka tuwe waaminifu, si wenye mafanikio. Kwa maneno mengine, tunaitwa kumpa Bwana kilicho bora zaidi tuwezacho, tukijitahidi kuwa waaminifu kwa mapenzi Yake matakatifu, kisha kumwachia yaliyobaki. Nyakati fulani inaweza kuonekana kwamba juhudi zetu zote hazizai matunda mema tunayoyatamani. Labda jaribio lako la kupatana na mtu mwingine halikufanikiwa. Au labda ulijitoa kwa moyo na roho katika kazi fulani ya kitume, lakini haikuonekana kamwe kustawi kama ulivyotarajia. Kuna uhuru mkubwa katika kutambua kwamba tunachoitwa kufanya ni kuwa waaminifu tu, si kuwa wenye mafanikio. “Mafanikio” hupimwa na Mungu, si kwa vigezo vya kibinadamu. Kwa kweli tunakuwa na “mafanikio” tu tunapokuwa waaminifu kwa mapenzi ya Mungu na wenye bidii katika kujitoa kwa kazi Yake ya kimungu. Tukiwa waaminifu kwa namna hii, hakuna kingine kilicho muhimu. Fanya kadiri ya uwezo wako wote na umwachie Mungu yaliyobaki (Tazama Shajara #1295).
Tafakari kiwango cha kujitoa kwako kwa Mapenzi ya Mungu. Kujitoa kwa Mapenzi matakatifu ya Mungu si sawa na kujifunga kufanikiwa kikamilifu katika yote unayofanya. Hata ikiwa kila unalofanya linaonekana kuishia katika kushindwa, unampendeza Mungu unapokuwa mwaminifu Kwake bila kuhangaikia matokeo. Mungu anauona moyo wako na anataka matendo yako mema yatolewe Kwake na kufanywa kulingana na Mapenzi Yake. Hakuna jambo jingine maishani lililo na umuhimu. Tanguliza uaminifu kuliko mafanikio, nawe utaufurahisha Moyo wenye huruma wa Bwana wetu.
Bwana, ninajitoa Kwako kwa ajili ya kukutumikia na kukutukuza. Ninajitolea kufanya yote unayoniita kufanya, na ninaomba niweze kutimiza mapenzi Yako kwa uaminifu na bidii. Unitumie, Bwana mpendwa, kama upendavyo, na unisaidie nikuachie yaliyobaki. Yesu, nakutumainia.
Tafakari 257: Mpango wa Mungu wa Muda Mrefu
Unapojitahidi kumtumikia Bwana wetu kwa moyo wako wote, unaweza kugundua kwamba anazungumza nawe kuhusu mapenzi Yake kwa kila siku. Huenda yasiwe wazi kabisa, lakini unaweza kuhisi kwamba anataka ufanye hili au lile. Kwa kawaida, Mungu hakuonyeshi kwa mara moja mpango mzima alio nao kwa ajili ya maisha yako. Badala yake, anakufunulia sehemu zake kidogo kidogo kadiri inavyohitajika. Kuamini kile anachokuita kufanya kila siku kunahitaji imani na kuitumainia sauti Yake ya upole. Ukweli ni kwamba Mungu anao mpango mkamilifu kwa ajili ya maisha yako, ikiwa tu utasikiliza na kuitikia hatua kwa hatua. Hatimaye, ukiwa Mbinguni, haya yote yataeleweka, nawe utaona hekima ya ajabu ya Bwana wetu. Hata hivyo, kwa sasa huenda usiweze kuuona mpango huo mpana kwa ukamilifu na uwazi. Hii ndiyo njia ya Mungu ya kukuvuta katika uhusiano wa kumtegemea na kujikabidhi Kwake kila siku. Jambo kuu ni kuwa mwaminifu kila siku kwa kile unachohisi Bwana wetu akisema. Ukifanya hivi, kidogo kidogo, mapenzi Yake matukufu yatafunuliwa maishani mwako, na kupitia wewe huruma Yake itamiminwa juu ya ulimwengu (Tazama Shajara #1300).
Unahisi Bwana wetu anakuita kufanya nini leo? Chochote kile, huenda usikielewe kikamilifu kwa sasa. Itumainie Sauti Yake ya upole na misukumo Yake leo, na ufuate mwongozo Wake. Fanya kile unachosikia akikuagiza. Ikiwa kile unachohisi kuwa ni Mapenzi Yake kinaonekana kisicho cha kawaida, zungumza na mtu mwingine kuhusu hilo ili uhakikishe kuwa kinatoka Kwake. Lakini hatimaye, ukijitahidi kutimiza Mapenzi Yake kila siku, utagundua kwamba njia anayokuongoza ni yenye utukufu na inatimiza kusudi Lake tukufu kwa maisha yako.
Bwana, ninatamani kukutumikia kwa moyo wangu wote. Unijalie neema ya kuwa na akili na moyo ulio wazi ili niweze kuitambua sauti Yako ya upole inayoniita kuishi kulingana na mapenzi Yako makamilifu. Maisha yangu ni Yako, Bwana mpendwa; unitendee kama upendavyo. Yesu, nakutumainia.
Tafakari 258: Ukaribu wa Mungu
Mungu yuko wapi? Ni rahisi kuwaza kwamba Mungu yuko Mbinguni au mahali fulani pa mbali, akitutazama kutoka juu na kuongoza uumbaji wote kulingana na mapenzi Yake matakatifu. Hii ni kweli, lakini si ukweli wote. Mungu “anapita mipaka yote” kikamilifu, kwa maana yuko juu yetu kwa mbali sana na juu ya ulimwengu ulioumbwa. Lakini pia “anakaa ndani” kikamilifu, kwa maana anaishi ndani yetu. Unaposali, mtafute hasa ndani ya nafsi yako mwenyewe. Kumbuka kwamba unapopokea Komunyo Takatifu, Mungu anaifanya nafsi yako kuwa tabernakulo. Anaingia na kubaki ndani, isipokuwa akiondolewa kwa sababu ya dhambi. Tafuta uwepo Wake wa kimungu ndani ya nafsi yako, nawe utagundua ukaribu wa huruma Yake tele (Tazama Shajara #1302).
Tafakari taswira ya tabernakulo. Ndani ya makao hayo matakatifu, utukufu wote wa Mungu umo ukiwa umesitiriwa. Lakini Yeye yupo humo, akiwa hai, aking’aa na akiwa na utukufu. Sasa itazame nafsi yako kama tabernakulo hiyo. Mwone akija kwako ili afanye makao Yake ndani yako. Mungu anatamani kuishi kikamilifu ndani yako, akiufanya moyo wako kuwa mahali pa pumziko Lake tulivu. Tenga muda leo kumtafuta Bwana wetu ndani yako. Zungumza Naye, msikilize, na uwe katika ushirika Naye. Uache moyo wako ujae uhai na kung’aa kwa uwepo Wake mtakatifu. Kwa maana ndani ya moyo wako umo uwepo wa Mungu.
Bwana, ninakushukuru kwa kuja kwangu na kuufanya moyo wangu kuwa makao Yako. Ninakushukuru kwa upendo Wako mkamilifu na kwa kunijali, nami ninaomba niweze kutambua uwepo Wako wa kimungu maishani mwangu kwa ukamilifu zaidi kila siku. Mimi ni Wako, Bwana mpendwa; iangazie nafsi yangu kwa utukufu Wako wa milele. Yesu, nakutumainia.
Tafakari 259: Uzuri wa Nafsi Nyenyekevu
Ni nini kinachomfanya mtu awe mzuri? Zaidi ya kitu kingine chochote, ni fadhila ya unyenyekevu. Unyenyekevu una mvuto wa pekee sana. Ingawa huenda baadhi ya watu wasivutiwe sana na mtu mnyenyekevu mwanzoni, baada ya muda unyenyekevu utamvuta hata mtu mwenye majivuno makubwa zaidi na anayejifikiria mwenyewe tu. Ni vigumu kupuuza mvuto wa kina wa mtu mnyenyekevu kwa sababu Mungu yupo ndani ya mtu huyo kwa ukaribu wa ndani kabisa. Kwa kweli, karibu tunaweza kusema kwamba Mungu angefanya chochote ambacho mtu mnyenyekevu anaomba. Ni kana kwamba unyenyekevu unamweka Mungu chini ya wajibu wa kujalia neema za pekee kupitia moyo wa mtu huyo mnyenyekevu. Unyenyekevu ni kujivua nafsi kikamilifu mbele ya Mungu na wengine. Matokeo yake ni kwamba mtu huyo “anatoweka” na anayebaki ni Mungu peke yake. Mungu anang’aa kupitia watu wanyenyekevu kwa mng’ao mkuu zaidi kuliko kupitia mtu mwenye vipawa vikubwa kuliko vyote. Jinyenyekeze mbele ya Mungu. Kadiri unavyojishusha, ndivyo Mungu anavyong’aa zaidi kupitia wewe na ndivyo Huruma Yake inavyojaliwa zaidi (Tazama Shajara #1306).
Je, unajitahidi kuwa mnyenyekevu? Au una mwelekeo wa kujitutumua na kutaka macho yote yaelekezwe kwako? Jambo la kushangaza ni kwamba, kama Maandiko yanavyosema, “Kwa maana kila anayejikweza atashushwa, lakini anayejinyenyekeza atakwezwa” (Luka 14:11). Watakatifu wengi wakuu ni mifano kamili ya jambo hili, kwa kuwa walijikita katika kumpenda Mungu na kuwapenda wengine, lakini hatimaye watakatifu hawa wakuu mara nyingi waliinuliwa juu ili wengine wawaone. Jitahidi kuwa mmoja wa watakatifu hao wakuu kwa kujinyenyekeza siku hii ya leo. Tafakari unyenyekevu na ujisadikishe kuhusu thamani yake. Kwa njia yake, uzuri na Huruma ya Mungu vitang’aa.
Bwana, najua kwamba nyakati fulani nimejaa kiburi na kwamba kiburi hicho kinanizuia kukiri ukweli huu. Tafadhali ninyenyekeze na unisaidie kujishusha mbele ya ukuu Wako usio na kikomo. Nijalie neema ya kukutafuta Wewe kuliko vitu vyote na kukupa utukufu na heshima yote. Yesu, nakutumainia.
Tafakari 260: Ukuu wa Matendo Madogo ya Upendo
Je, unatamani kufanya mambo ya ajabu katika ulimwengu huu? Je, nyakati fulani una mawazo na ndoto kubwa sana? Wakati mwingine tuna ndoto za kidunia zaidi za utajiri na umaarufu, na wakati mwingine tunaweza kuwa na ndoto za kufanya mambo ya pekee kwa ajili ya Mungu na Kanisa. Lakini si lazima mambo hayo yabaki kuwa ndoto, kwa sababu kila mmoja wetu ameitwa kufanya mambo ya pekee. Tatizo ni kwamba mara nyingi hatuelewi vizuri maana ya “mambo ya pekee.” Basi maana yake ni nini? Hasa ni kufanya mambo madogo kwa upendo wa pekee. Kila mmoja wetu anaweza kufanya hivi kila siku, siku nzima. Maisha yetu yamejaa nafasi za kufanya “mambo madogo.” Huenda ikawa kupika au kufanya usafi, kuwapeleka watoto huku na kule, kutunza ua wa nyumbani, kukamilisha majukumu kazini, au mazungumzo ya kawaida ya kila siku na wengine. Kila moja ya shughuli hizi inatupa nafasi ya kupenda kwa upendo wa pekee. Na ukifanya kila tendo dogo kwa upendo mkubwa, basi upendo wako utakuwa mkubwa na Mungu atafanya mambo ya pekee kupitia maisha yako, akiwajalia wengi Huruma Yake (Tazama Shajara #1310).
Fikiria mambo madogo unayopaswa kufanya leo. Unawezaje kufanya kazi hizi rahisi kwa upendo wa pekee? Mambo mengi tunayofanya huyafanya bila kupenda au bila kujali. Tunaweza kushindwa kuona thamani katika shughuli ndogo za kila siku zinazojirudia bila mabadiliko. Hili ni kosa. Tafuta njia za kufanya kila jambo kama tendo la upendo na kama sadaka kwa Mungu. Tenda kwa moyo wa ibada na kwa makusudi katika kila fursa unayopata, na ndoto zako za kufanya mambo makubwa zitatimia kwa sababu ya Huruma ya Mungu inayong’aa kupitia maisha yako.
Bwana, leo ninakutolea kila tendo dogo ninalofanya. Nisaidie kuona thamani na maana hata katika huduma ndogo kuliko zote. Ninaomba upendo wangu Kwako uongezeke kwa njia ndogo zisizohesabika ili niwe chombo kitakatifu cha Huruma Yako tele. Yesu, nakutumainia.
Tafakari 261: Yesu Aliyejificha Ndani ya Wengine
Hebu fikiria kama Yesu angekujia akiwa maskini, mwenye njaa na anayeteseka kwa baridi, akakuomba umtunze. Tukio hili lingeweza kukushtua na kukufanya ujiulize ikiwa mtu huyu alikuwa Yesu kweli. Lakini ni Yesu. Yesu anatujia kila siku katika mtu mwenye uhitaji. Huenda tukakutana na mtu asiye na makazi, mwenye njaa na anayehitaji mavazi. Ikiwa hali ni hiyo, basi huyu ni Yesu. Lakini kuna watu wengi tunaokutana nao kila siku ambao wana njaa na kiu za aina nyingine. Wengi wana njaa kali ya upendo, kueleweka, huruma na kujaliwa. Kwa nje wanaweza kuonekana wasiokaribisha wengine, lakini ndani wao ni Bwana wetu, anayetafuta kupokea huruma kutoka moyoni mwako. Usisite kumwona Bwana wetu akiwa katika kila mtu unayekutana naye. Wamiminie huruma ya moyo wako, hasa mtu wa kusikitikiwa zaidi, nawe utakuwa umemmiminia upendo wako Yesu mwenyewe (Tazama Shajara #1312).
Je, unawatendeaje maskini na ombaomba? Anza kwa kuwafikiria wenye mahitaji ya kimwili, lakini tafakari kwa kina zaidi ili kuwafikiria wote wenye mahitaji mengine. Wafikirie wenye mioyo migumu, wenye dhambi, wenye kiburi, wenye majivuno, watu waliojaa hasira, na kadhalika. Kila mtu unayemkumbuka ni Bwana wetu anayekujia ili aonje huruma ya moyo wako. Chochote unachomfanyia aliye mdogo kuliko wote kati ya hawa, unamfanyia Kristo. Je, unaamini hili? Ikiwa unaamini, basi imani hii lazima ionekane kwa vitendo kwa wewe kumwonyesha huruma kila mtu, hasa wale unaoona kuwa ni vigumu zaidi kuwapenda. Tafakari swali hili la vitendo leo na uazimie kumtafuta Bwana wetu katika “ombaomba” mwingine utakayekutana naye, hata kama anaonekana kuwa mtu usiyetaka kuwa karibu naye hata kidogo.
Bwana, ninakupenda na ninatambua kwamba lazima nikutafute katika kila mtu ninayekutana naye. Nipe macho ya kukuona na moyo wa kukupenda. Ninapokupenda katika wengine, Bwana mpendwa, ruhusu huruma iliyo moyoni mwangu ikupe furaha tamu. Yesu, nakutumainia.
Tafakari 262: Utawala wa Upendo au Haki
Hatuwezi kuukwepa Mkono wa Mungu. Yeye ndiye anayeutegemeza ulimwengu na kudumisha uwepo wa vitu vyote. Bila utunzaji Wake wa daima tungekoma kuwepo. Lakini tunabaki chini ya Mkono wa maongozi Yake kwa mojawapo ya njia mbili. Ama tunaongozwa na “utawala wa upendo” au na “utawala wa haki.” Utawala wa haki ni njia ya Mungu ya kuyaongoza maisha yetu tunapomgeukia kisogo. Hatuwezi kuikwepa haki Yake hapa duniani wala wakati wa kufa. Tunapotenda dhambi, hasa kwa namna nzito, tunakuwa watumwa wa dhambi yetu kutokana na haki ya Mungu. Anatuacha tuonje kifungo cha dhambi kwa sababu ya Huruma Yake kuu. Hii ni Huruma kwa kuwa athari chungu za haki Yake zinawekwa juu yetu ili kutuita tutubu. Lakini wale wanaoishi chini ya utawala wa upendo wamebarikiwa kuishi katika kiwango kipya kabisa cha maisha. Nafsi hizi takatifu zinafurahia Huruma ya Mungu na zinawekwa huru kutoka katika athari za dhambi. Zinaonja matunda mengi ya Roho na kutenda kulingana na Mapenzi matakatifu ya Mungu (Tazama Shajara #1315).
Unaishi chini ya utawala upi? Je, mara kwa mara unapoteza neema na kukumbana na haki ya Mungu maishani mwako? Au unajitahidi kuishi chini ya utawala Wake wa upendo? Popote ulipo leo, jua kwamba hiyo ni zawadi ya Huruma ya Mungu. Ruhusu haki Yake iyaelekeze upya maisha yako unapoanguka, na ujitahidi kuupokea umiminiko wote wa Huruma Yake. Bwana hatakuacha kamwe, lakini namna utakavyoionja Huruma Yake inategemea wewe.
Bwana wangu, ninatamani kujazwa na uwepo Wako wenye huruma maishani mwangu. Ninaomba kwamba kila siku niache dhambi yangu na kuonja uhuru na furaha inayotokana na kuishi chini ya utawala Wako wa upendo. Unisaidie, Bwana mpendwa, kufanya daima maamuzi yaliyo sahihi maishani mwangu ili nivutwe kuingia katika uzima tele ulioniandalia. Yesu, nakutumainia.
Tafakari kuhusu Daftari la Tano: 263-326
Pia Kinapatikana kama Kitabu cha Kielektroniki & Kitabu chenye Jalada Laini

Amazon – Barnes and Noble – Google Play – iTunes
