Kiswahili

Utangulizi

Dunia tunamoishi leo ni dunia yenye vurugu, machafuko, kukata tamaa na upweke wa ndani vinavyozidi kuongezeka.  Ni dunia ambamo watu wengi sana wameunganishwa kupitia njia za kisasa za mawasiliano, kama vile vichwa vya habari vya kila siku na mitandao ya kijamii.  Kwa hiyo, tunazidi kufahamu matatizo na majanga yasiyohesabika ambayo watu wengi sana wanakabili kila siku.  Kwa watu wengi sana, majanga haya yanazidi kuwa chanzo cha udadisi wa kudumu, kuridhika, na hata kuyafuatilia kwa namna inayotawala kabisa mawazo yao.

Kutokana na kukabiliwa daima na habari za matatizo ya kushtua katika ulimwengu wetu, kila siku tunavutwa katika matukio yenye uchungu ya ulimwengu ulioanguka dhambini.  Tunaona dhambi na matokeo yake kila tunapotazama, na hali hiyo inazichosha nafsi zetu.

Basi, tunakabilianaje na hali hii ya kufahamu daima maovu, dhambi na maumivu ya watu wengi namna hii?  Jibu pekee ndilo kiini cha kitabu hiki: Huruma ya Mungu.

Huruma ya Mungu lazima iwe kama lenzi ambayo kupitia hiyo tunavitazama vitu vyote.  Lazima iwe kichujio cha kila tunachopokea na kila tunachotoa.  Huruma ya Mungu inahitajika sana leo, nasi tunaweza kuwa na hakika kwamba Yeye aliye Mungu anatamani kutujalia zawadi hii ya thamani kwa wingi.

Huruma ni nini?  Kwa namna ya pekee zaidi, Huruma ya Mungu ni nini?  Huruma ya Mungu ni neema na upendo wa Mungu ulio hai katika maisha yetu.  Ni Mungu akitenda kazi ndani yetu, juu yetu na kupitia sisi.  Ni Mungu akiyaongoza maisha yetu na kutufundisha jinsi ya kufikiri na jinsi ya kutenda.  Ni Mungu akitutwaa tuwe Wake ili tusitawaliwe na wazimu wa ulimwengu tunamoishi.

Huruma ya Mungu ni kama chemchemi ya maji yasiyokoma katikati ya jangwa kame lililokauka kabisa.  Ni chemchemi ya burudisho na upya wa maisha ambayo sisi sote tunaitafuta, iwe tunatambua au la.  Ndiyo shauku ya ndani kabisa ya mioyo yetu, na ndiyo pekee inayoweza kutosheleza kabisa shauku tuliyo nayo.

Ulimwengu tunamoishi hujaribu kuturidhisha na kututosheleza kwa vichocheo vya daima, misisimko, matukio ya kuvuta hisia na mambo yenye kuvuta udadisi.  Ulimwengu hutupatia daima hisia za uongo za furaha na utimilifu.  Hatua ya kwanza ya kuigundua Huruma ya Mungu ni kuuona ulimwengu jinsi ulivyo.  Ni kuona uongo na udanganyifu unaotuzunguka na kuelekeza macho yetu kwenye chemchemi hii ya ukweli na neema ambayo tuliumbwa kwa ajili yake.  Tunahitaji kuielekea Huruma ya Mungu.

Kama chemchemi ya neema inayobubujika mahali pakame, Huruma ya Mungu hutoka katika chanzo kilichofichika, huendelea kutiririka bila kuisha kamwe, na hutupatia yote tunayohitaji ili kupata uradhi maishani.  Ni kama bahari kubwa sana ambayo tunaitwa kujitosa ndani yake na kuzama katika vilindi vyake.  Haina mwisho na hutuzunguka na kutujaza kabisa.

Yesu daima ametupa mifano ili kujaribu kueleza upendo alio nao kwetu. Yeye ni Baba mwenye upendo, anayemngojea mwanawe aliyepotoka arudi.  Yeye ni Mchungaji Mwema anayemtafuta kondoo mmoja aliyepotea.  Yeye ni Msamaria Mwema aliyemhudumia mgeni aliyekuwa katika shida kubwa.

Bila shaka, mifano hii haiwezi kamwe kueleza kikamilifu kina cha Huruma Yake na upendo Wake. Kila mfano huwa na maana yake kwa kila mtu kulingana na uzoefu na historia yake binafsi.  Zawadi moja ambayo Mungu ametujalia katika nyakati za karibuni ni Sista Maria Faustina Kowalska.  Alizaliwa tarehe 25 Agosti 1905 huko Kraków, Poland, na alifariki tarehe 5 Oktoba 1938 katika mji huohuo akiwa na umri wa miaka thelathini na mitatu.  Akiwa bado kijana wa miaka ishirini, alijiunga na Shirika la Masista wa Bikira Maria wa Huruma huko Warsaw, na baadaye alihamishiwa Płock kisha Vilnius.  Huko Vilnius ndiko alikokutana na muungamishi wake, Padre Michał Sopoćko, aliyemsaidia sana kuhusu neema nyingi za kimistiki alizopokea kutoka kwa Mungu.  Sista Faustina alijaliwa neema ya kupokea kila siku mafunuo binafsi kutoka kwa Yesu, ambayo kwa hayo alimfunulia wingi wa Huruma Yake ya Kimungu.

Kwa maelekezo ya mkuu wake, Padre Sopoćko na Yesu Mwenyewe, aliandika shajara ya mang’amuzi haya ya kimafumbo, ambayo leo inajulikana kama Huruma ya Mungu Ndani ya Nafsi Yangu: Shajara ya Mtakatifu Maria Faustina Kowalska.

Lengo la kitabu hiki ni kupitia kurasa za Shajara yake, tukitafakari ujumbe wake katika kipindi cha mwaka mmoja.  Shajara inatafakariwa kwa namna ambayo itamwezesha msomaji kutafakari kwa urahisi ujumbe wa Huruma ya Mungu kama ulivyofunuliwa kwa Sista Faustina na Yesu Mwenyewe.

Tarehe 30 Aprili 2000, Papa Yohane Paulo II alimtangaza Sista Faustina kuwa mtakatifu katika Jumapili ya Huruma ya Mungu.  Kufuatia kutangazwa kwake kuwa mtakatifu, ujumbe wa Mtakatifu Faustina unaendelea kuenea katika dunia yenye uhitaji mkubwa sana wa neema tele ya Mungu.

Tarehe 8 Desemba 2015, Papa Fransisko alianza Jubilei Maalumu ya Huruma kwa ajili ya Kanisa na dunia.  Kitabu hiki ni tunda la Mwaka huo wa Huruma na kiliandikwa katika Mwaka huo wa Jubilei ili kumsaidia kila mtu anayesoma kurasa zake kuingia kwa undani zaidi katika Huruma ya Mungu kwa miaka ijayo.

Yaliyomo

Muundo wa Kitabu Hiki

Utangulizi kwa Mapadre

Tafakari: 1-10


Pia Kinapatikana kama Kitabu cha Kielektroniki & Kitabu chenye Jalada Laini

Huruma ya Mungu

Amazon – Barnes and Noble – Google Play – iTunes